National News

WAHITIMU WA KIDATO CHA NNE WATAKIWA KUJIEPUSHA NA UHALIFU

Tarehe: 30 Oct, 2026


Wahitimu wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari ya Kinyaka, iliyopo Kata ya Nyamnyusi, Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, wametakiwa kujiepusha na vitendo vya uhalifu na badala yake kuzingatia maadili mema, uzalendo na kuwa raia wema wanaochangia maendeleo ya jamii.


Wito huo umetolewa Oktoba 29, 2026, na Polisi Kata ya Nyamnyusi, Willy Lupa, wakati akizungumza na wahitimu hao kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria, kulinda amani na usalama katika jamii, pamoja na kuepuka makundi yanayoweza kuwashawishi kujihusisha na vitendo vya uhalifu.

Lupa amewataka wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kujenga maisha yenye nidhamu na uwajibikaji, huku akiwahimiza kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani katika maeneo yao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kinyaka, Reuben Daud, amesema kuwa wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa wakijengewa misingi ya nidhamu, uzalendo na maadili mema, akieleza kuwa anaamini wahitimu hao wataendelea kuzingatia misingi hiyo na kuwa raia wema wenye mchango chanya katika maendeleo ya jamii.

Nao, baadhi ya wahitimu wa shule hiyo wameahidi kuwa mabalozi wa amani kwa kuwaelimisha vijana wenzao wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kuhusu umuhimu wa kuachana na tabia hizo, huku wakieleza kuwa wataendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa kwa wakati wanapobaini viashiria vya uhalifu na uvunjifu wa amani katika maeneo yao.