Wananchi wa Kata ya Nyansha, iliyopo Halmashauri ya Mji wa Kasulu, mkoani Kigoma, wameeleza kutoridhishwa na ongezeko la bei ya maji, kutoka shilingi 300 hadi shilingi 1,109 kwa unit moja, wakieleza kuwa ongezeko hilo linaweza kuongeza gharama za maisha na kufanya huduma ya maji kuwa mzigo kwa baadhi ya kaya.
Wakitoa maoni yao katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kasulu (KUWSSA), kwa lengo la kutambulisha bei mpya za maji, uliofanyika Oktoba 26, 2026, wananchi hao wamesema ongezeko hilo ni kubwa na linahitaji maelezo ya kina, huku wakihofia athari zake katika uwezo wa wananchi kumudu gharama za huduma hiyo muhimu.
Akijibu hoja za wananchi, Meneja wa Usambazaji Maji wa KUWSSA, Goodluck Shefatia, amesema ongezeko la bei limelenga kukidhi gharama za uboreshaji wa miundombinu ya maji, kulipa wafanyakazi pamoja na kuimarisha ubora wa huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Nyansha, Lameck Anthony Lukole, amewataka wananchi kuwa watulivu na kuelewa sababu za mabadiliko hayo, akieleza kuwa bei hizo zimepitishwa na wataalamu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kwa lengo la kuwezesha utoaji wa huduma ya maji kwa ufanisi na ubora zaidi.
Kwa mujibu wa tangazo lililochapishwa katika Gazeti la Serikali la Oktoba 16, 2026, bei mpya za maji kwa watumiaji wa nyumbani zimeongezeka kutoka shilingi 300 hadi shilingi 1,109 kwa unit, huku kwa taasisi zikiongezeka kutoka shilingi 400 hadi shilingi 1,479, watumiaji wa kibiashara sasa watalipa shilingi 1,885 kwa unit, kutoka shilingi 510 za awali, wakati bei kwa watumiaji wa maji kupitia vioski imeongezeka kutoka shilingi 400 hadi shilingi 1,475 kwa unit.
Ongezeko hilo limeibua mjadala miongoni mwa wananchi kuhusu gharama za upatikanaji wa huduma ya maji, huku wakitarajia kuwa mamlaka husika itaendelea kutoa ufafanuzi na kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa ubora na kwa gharama zinazoweza kumudu na wananchi.