National News

UPANUZI WA ZAHANATI YA KITEMA WAPUNGUZA ADHA KWA WANANCHI

Tarehe: 29 Oct, 2026


Changamoto ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya kwa wakazi wa Kijiji cha Kitema na maeneo jirani wilayani Kasulu, imepungua kufuatia upanuzi wa zahanati ya kijiji hicho uliogharimu Sh milioni 222.1, fedha zilizotolewa na serikali kupitia uwekezaji wa afya ya mama na mtoto katika mwaka wa fedha 2024/2025.


Wakizungumzia uboreshwaji wa huduma hiyo, wakazi wa kijiji cha Kitema na Mketa wamesema upanuzi wa zahanati hiyo umeleta nafuu kubwa kwa wananchi kwa kuwa sasa wanapata huduma katika mazingira bora zaidi, huku wakieleza kuwa ujenzi wa nyumba za watumishi umechangia kuboresha upatikanaji wa huduma kwa kuwa watumishi wanaishi karibu na kituo cha afya na hivyo kuwa rahisi kuwafikia wananchi wanapohitaji msaada.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kitema, Abraham Ntebanyi, amesema uwepo wa kliniki ya Baba, Mama na Mtoto pamoja na upanuzi wa chumba cha kujifungulia umeboresha mazingira ya utoaji wa huduma na kupunguza changamoto zilizokuwapo awali.

Akifafanua kuhusu mradi huo, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kitema, Ezikiel Lawrence, amesema fedha hizo zilitumika kujenga nyumba mbili za watumishi, kliniki ya Baba, Mama na Mtoto na jengo la kujifungulia, pamoja na kupanua jengo la wagonjwa wa nje (OPD).

Amesema utekelezaji wa mradi ulianza Novemba 21, 2025 na umekamilika kwa asilimia 100, ambapo ameeleza kuwa upanuzi wa eneo la kujifungulia umechangia kuongeza idadi ya wajawazito wanaochagua kujifungulia kituoni badala ya nyumbani, kufuatia kuboreshwa kwa miundombinu na mazingira ya huduma.

Awali, wakazi wa Kitema walilazimika kusafiri hadi Nyamunyusi na Kabanga kufuata baadhi ya huduma za afya, hali iliyokuwa ikiongeza usumbufu kwa wananchi na changamoto kwa wajawazito waliokuwa wakihitaji huduma za kujifungua.