National News

SIRRO AAGIZA KUIMARISHA MAANDALIZI YA KUKABILIANA NA ATHARI ZA EL NINÕ

Tarehe: 29 Oct, 2026


Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro amewataka viongozi wa Serikali, taasisi binafsi pamoja na watendaji wa kata, mitaa na vijiji kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuwajibika ipasavyo katika kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño. 


Balozi Sirro amesema hayo, wakati akizungumza katika kikao cha maandalizi na utayari wa kukabiliana na athari hizo kilichofanyika katika Halmashauri ya Mji Kasulu, ambapo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa viongozi na wadau wote katika kuhakikisha hatua za kinga na tahadhari zinatekelezwa kwa wakati, kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya changamoto za hali ya hewa, kusafisha mifereji, mitaro pamoja na kutekeleza maazimio ya kikao hicho. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Luteni Kanali Joseph Murimi, ameeleza hatua mbalimbali zilizochukuliwa ndani ya Wilaya hiyo ikiwemo Halmashauri ya Mji Kasulu ambapo tayari maeneoe hatarishi yameshatambuliwa, Elimu kwa wananchi imeanza kutolewa na zoezi la kusafisha mifereji na mitaro likiwa bado linaendelea. 

Viongozi wa Serikali kutoka wilaya zote za Mkoa wa Kigoma wamewasilisha na kusoma taarifa mbele ya Mkuu wa Mkoa, zikielezea mipango na mikakati iliyowekwa kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño katika maeneo yao.