WANANCHI MURUVUMU B WACHANGISHANA FEDHA KUKARABATI CHEMICHEMI
Tarehe: 10 Oct, 2026
Wananchi wa Mtaa wa Muruvumu B, Kata ya Kimobwa, Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma, wameweka mikakati ya kuchangishana fedha kwa ajili ya kukarabati chemichemi ya Kihomoka, ambayo imeharibika kwa muda mrefu, ili kuboresha huduma ya maji kwa wananchi.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika mtaani humo, uliolenga kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo huduma za afya, miundombinu pamoja na ulinzi na usalama wa mtaa.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Muruvumu B, Jackson Musuguru, amewataka wananchi kupendekeza kiasi cha fedha ambacho kila kaya inaweza kuchangia ili kuwezesha ukarabati wa chemichemi hiyo, ambapo ameeleza kuwa baada ya kufikia makubaliano kuhusu kiwango cha uchangiaji, uongozi wa mtaa utawasilisha maombi ya kibali cha kuchangisha fedha katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wamependekeza kila kaya kuchangia shilingi elfu nne na mia tano, wakieleza kuwa kiwango hicho kinaweza kusaidia kugharamia ukarabati wa chemichemi hiyo.
Hatua hiyo inalenga kuwezesha wananchi kupata huduma ya maji kupitia chemichemi ya Kihomoka, huku ushirikiano kati ya wananchi na uongozi wa mtaa ukitajwa kuwa muhimu katika kufanikisha juhudi hizo za maendeleo.