MAAFISA UGANI TOKENI OFISINI MKAWASIAIDIE WAKULIMA NA WAFUGAJI- RC SIRRO
Tarehe: 01 Aug, 2026
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amewataka maafisa ugani kuwafikia wafugaji na wakulima ili kuwapatia Elimu itakayowawezesha kufanya Kilimo cha kisasa kitakachohusisha matumizi ya Teknolojia na kuzalisha kwa tija.
Akifungua Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Magharibi katika viwanja vya Ipuli mkoani Tabora, Balozi Sirro amesema makundi hayo yanapaswa kutumia maarifa wanayopata kutoka kwa wataalam ili kuongeza tija, ubora wa bidhaa na uzalishaji unaokidhi mahitaji ya soko.
Amesema wananchi wanapaswa kubadili mitazamo yao na kuaminika kuwa shughuli za Kilimo na ufugaji ni miongoni mwa kazi zenye faida na zinazoweza kuwainua kiuchumi na kubadilisha maisha yao Katika hatua nyingine Balozi Sirro amezitaka Halmashauri kupitia wataalam wake, kuendelea kuhamasisha wananchi kujikita katika ufugaji wa Nyuki, ufugaji Samaki kwa vizimba sambamba na wajasiriamali kupatiwa ujuzi wa usindikaji bora wa bidhaa zao.
“Wataalam hakikisheni mnayatembelea makundi hayo badala ya kusubiri waje kwenye maonesho hapa, kwani wanaoshiriki ni wachache ikilinganishwa na idadi halisi” amesisitiza Balozi Sirro.
Sambamba na hayo Mkuu huyo wa Mkoa, amehimiza matumizi ya teknolojia katika maonesho hayo ili kuleta chachu kwa wakulima kujifunza ujuzi mpya na kutumia maarifa wanayoyapata kuongeza uzalishaji.