National News

MWENGE WAZINDUA MITA ZA MAJI ZA PREPAID MANISPAA YA KIGOMA UJIJI

Tarehe: 14 Sep, 2026


Mita mpya za maji za mfumo wa Prepaid zaidi ya 100 zenye thamani ya Shilingi milioni 39.5 zimezinduliwa katika Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma, hatua inayolenga kuwawezesha wananchi kulipia huduma ya maji kabla ya matumizi na kupunguza migogoro ya bili za maji.


Mita hizo zimezinduliwa katika Manispaa ya Kigoma Ujiji wakati wa ziara ya Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, ambapo Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini Clayton Chipando, maarufu Baba Levo, wananchi na viongozi wa Manispaa hiyo wameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa maboresho hayo, huku wakiahidi kutunza miundombinu hiyo.

Mfumo huo wa Prepaid unatarajiwa pia kuwasaidia wananchi kufuatilia matumizi yao ya maji na kupunguza malalamiko yanayohusiana na ubambikizaji wa bili.

Katika hatua nyingine, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Ndg. Wazo Michael Mwang'onda, ameipongeza Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa kuvuka lengo la usajili wa makundi ya wananchi kwa ajili ya kupata zabuni.

Amesema Mwenge wa Uhuru ulilenga kusajili makundi 150, lakini Manispaa hiyo imefanikiwa kusajili makundi 210 na kutoa zabuni zenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 1.05.

Akizungumza na wananchi katika uwanja wa Mwanga Community Center, Mwang'onda amesema Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa sasa inashika nafasi ya kwanza miongoni mwa Halmashauri zote ambazo Mwenge wa Uhuru umepita katika mikoa 26, huku ikishindana na majiji makubwa nchini.

Amesema kwa sasa Manispaa hiyo inatanguliwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha, ikifuatiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Awali, taarifa iliyotolewa na Manispaa ya Kigoma Ujiji kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii na Idara ya Ununuzi wa Umma, imeeleza kuwa Manispaa hiyo ina dhamira ya kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma, kwa lengo la kuwawezesha wananchi wenye hali ya chini kiuchumi.

Makundi yanayolengwa kunufaika na fursa hizo ni pamoja na wazee, wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mbali na mita hizo za maji, Mwenge wa Uhuru pia umezindua miradi mbalimbali katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, ikiwemo maeneo ya biashara na bweni la wanafunzi katika Shule ya Sekondari Buronge.