Polisi Kasulu Wawafariji Wagonjwa wa Wodi ya Wazazi kwa Msaada wa Zawadi
Tarehe: 31 Jul, 2026
Jeshi la Polisi Wilaya ya Kasulu limetoa zawadi mbalimbali kwa wagonjwa wanaopatiwa huduma katika Wodi ya Wazazi ya Hospitali ya Mji wa Kasulu, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu wake wa kijamii na juhudi za kuimarisha uhusiano na ushirikiano na wananchi.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi hizo, Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kigoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi Alfred Kasoro, alisema Jeshi la Polisi linaendelea kushiriki shughuli za kijamii zinazolenga kuwasaidia wananchi wenye uhitaji na kuchangia ustawi wa jamii.
Alisema msaada huo unalenga kupunguza baadhi ya changamoto zinazowakabili wagonjwa na familia zao, huku ukiendelea kujenga imani na ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, jambo ambalo pia husaidia katika kuzuia na kupambana na uhalifu.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Kasulu, ambaye pia ni Muuguzi Mfawidhi wa hospitali hiyo, Editha Yohana, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa msaada huo, akisema utawasaidia wagonjwa kukidhi baadhi ya mahitaji muhimu wanapokuwa hospitalini na kupunguza sehemu ya mzigo wa gharama kwa familia zao.
Baadhi ya wagonjwa walionufaika na msaada huo wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo, wakisema imewapa faraja na kuwahakikishia kuwa bado jamii inawajali katika kipindi chao cha matibabu. Pia wameomba Jeshi la Polisi kuendelea na shughuli za kijamii zinazolenga kuimarisha mshikamano na ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya usalama.