TFF Yaondoa Kipengele cha Kudhibiti Wachambuzi wa Soka kwenye Kanuni
Tarehe: 30 Jul, 2026
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, amesema kipengele kilichokuwa kinapendekezwa kuhusu udhibiti wa wachambuzi wa soka hakitakuwa sehemu ya kanuni za shirikisho baada ya kuondolewa katika rasimu ya mwisho.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi, Julai 30, 2026, katika Makao Makuu ya TFF, Karume jijini Dar es Salaam, Karia amesema kipengele hicho kilitokana na mapendekezo yaliyowasilishwa na baadhi ya wadau wa klabu wakati wa mchakato wa kuandaa kanuni hizo.
Amesema baada ya kupitia mapendekezo hayo, TFF ilibaini kuwa usimamizi wa wachambuzi wa soka haupo ndani ya mamlaka ya shirikisho, bali unasimamiwa na sheria za nchi pamoja na mamlaka nyingine husika.
"Lilikuwa ni pendekezo kutoka kwa wadau, lakini tulibaini kuwa suala la wachambuzi wa soka linasimamiwa na sheria za nchi pamoja na mamlaka nyingine husika, hivyo tukaliondoa," amesema Karia.
Karia amesisitiza kuwa TFF haina jukumu la kusimamia au kudhibiti wachambuzi wa soka, hivyo haikuwa sahihi kulijumuisha suala hilo katika kanuni za shirikisho.