Madiwani Kasulu Watakiwa Kutoa Mrejesho Kwa Wananchi Kuhusu Miradi ya Maendeleo
Tarehe: 30 Jul, 2026
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, wametakiwa kuhakikisha wanatoa mrejesho kwa wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika kata zao, hatua inayolenga kuimarisha uwazi, ushirikishwaji wa wananchi na kuongeza imani kwa Serikali.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu, Bi. Teresia Mtewele, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo katika kikao cha Baraza la Madiwani la robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026, kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.
Bi. Mtewele amesema kuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaendelea katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, hivyo ni wajibu wa madiwani kuwafahamisha wananchi hatua za utekelezaji wa miradi hiyo, mafanikio yaliyopatikana pamoja na manufaa yanayotarajiwa, ili kuongeza uwajibikaji na ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Kasulu, Mapigano Francis, akimwakilisha Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo, amewataka madiwani kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira, ikiwemo kuhifadhi misitu na kudhibiti uharibifu wa mazingira, ili kulinda vyanzo vya maji na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Akihitimisha Baraza hilo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Charles Benjamin, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na Serikali katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo, hususan ukusanyaji wa mapato ya ndani, akisema hatua hiyo itaiwezesha halmashauri kuendelea kuboresha huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi ya wilaya hiyo.