National News

Binti wa Miaka 16 Akamatwa kwa Tuhuma za Kumuua Mama Yake Pwani

Tarehe: 30 Jul, 2026


Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia binti mwenye umri wa miaka 16 kwa tuhuma za kumuua mama yake mzazi, Hadija Shaha (51), kufuatia ugomvi unaodaiwa kuzuka baada ya kuzuiwa kuhudhuria sherehe ya siku ya kuzaliwa ya rafiki yake.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi, Julai 30, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salum Morcase, amesema tukio hilo lilitokea usiku wa Julai 28, 2026, katika Kijiji cha Msoga, Wilaya ya Chalinze.

Kamanda Morcase amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa marehemu, ambaye alikuwa na ulemavu wa miguu yote miwili, alimzuia binti huyo kwenda kwenye sherehe ya siku ya kuzaliwa ya rafiki yake iliyokuwa ikifanyika karibu na Hospitali ya Msoga.

Amesema baada ya kuzuiwa, ugomvi ulizuka kati yao na inadaiwa kuwa binti huyo alimshambulia mama yake kwa kutumia kitu chenye ncha kali, na kusababisha majeraha yaliyosababisha kifo chake.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa kwa ajili ya uchunguzi, huku likisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa mara baada ya uchunguzi kukamilika.