National News

Serikali Kigoma Yasema Mradi wa Buhoma Umeboresha Elimu na Maisha ya Wananchi

Tarehe: 30 Jul, 2026


Serikali ya Mkoa wa Kigoma imepongeza mchango wa wadau wa maendeleo kwa kuimarisha sekta ya elimu na maendeleo ya jamii kupitia utekelezaji wa Mradi wa Maendeleo ya Jamii wa Buhoma katika Wilaya ya Kasulu.


Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma katika hafla ya kufunga rasmi mradi huo iliyofanyika Kijiji cha Kalimungoma, Kata ya Makere.

Kanali Mwakisu amesema wadau wa maendeleo wamekuwa washirika muhimu wa Serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi kupitia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu, pamoja na utoaji wa vifaa na nyenzo mbalimbali za kujifunzia, hatua zilizochangia kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika maeneo yaliyofikiwa na mradi huo.

"Ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo kama World Vision umeendelea kuleta matokeo chanya katika sekta ya elimu na kuboresha maisha ya wananchi," amesema Mwakisu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika hilo, Steven Nyagonde, amesema mafanikio ya Mradi wa Buhoma yametokana na ushirikiano mzuri kati ya shirika hilo, Serikali, wafadhili na wananchi, ambao kwa pamoja wamefanikisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika jamii.

Nyagonde amewashukuru wadau wote walioshiriki kufanikisha mradi huo na kueleza kuwa mafanikio yaliyopatikana ni uthibitisho wa nguvu ya ushirikiano katika kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi.

Nao baadhi ya wananchi wa Kata ya Makere wameeleza kuwa miradi iliyotekelezwa na World Vision imeleta mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu, huduma za kijamii na ustawi wa maisha yao. Wamesema wanatarajia ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo utaendelea ili kudumisha na kuongeza mafanikio yaliyopatikana kupitia Mradi wa Buhoma.