WAZIRI KATAMBI AFUNGUKA KUHUSU WATU 130 WALIOKAMATWA
Tarehe: 29 Jul, 2026
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema watu 130 waliokamatwa kwa tuhuma za makosa mbalimbali ni watuhumiwa na si viongozi au wahadhiri, akisisitiza kuwa hakuna mtu, kikundi au taasisi iliyolengwa katika hatua hizo.
Katambi amesema hayo leo Julai 29, 2026 visiwani Zanzibar, wakati akitoa ufafanuzi kuhusu malalamiko yaliyojitokeza kufuatia kukamatwa kwa watuhumiwa hao, ambapo amesema Serikali inatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria bila kulenga mtu au taasisi yoyote.
Amesema Tanzania iko salama na imara katika kukabiliana na matukio ya uvunjifu wa amani, huku akieleza kuwa hakuna sababu ya kutetea jambo ambalo halijafahamika kwa kina, hasa kwa kuwa baadhi ya mashauri yako mahakamani.
“Hakuna mtu ambaye anaweza kulengwa wala hakuna kusudio lolote linalokusudia kumlenga mtu au taasisi. Kama ingekuwa kuna lengo maalumu, mbona kuna wanataaluma wengi wako huru? Kwa hiyo tusitetee vitu ambavyo hatuvijui, hasa kwenye mashauri ambayo yako mahakamani kwa sasa hatuna ujasiri wa kuyahoji. Uganda Convention sio kinga ya jinai,” amesema Waziri Katambi.
Ameongeza kuwa hatua za kisheria zinazochukuliwa na Serikali zinalenga kuhakikisha sheria inazingatiwa na kulinda amani na usalama wa nchi.