YANGA YAINASA SAINI YA PETER SHALULILE WA MAMELOD SUNDOWNS
Tarehe: 28 Jul, 2026
Klabu ya Yanga imefanikiwa kunasa saini ya mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Namibia, ambaye Juni 2, 2026 mkataba wake na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ulimalizika baada ya kuhudumu kwenye kikosi cha Masandawana kwa miaka sita, akiweka rekodi kibao barani Afrika.
Shalulile aliondoka Mamelodi Sundowns akiwa ameisaidia klabu hiyo kutwaa mataji mbalimbali, ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika ya CAF (TotalEnergies CAF Champions League) na African Football League, huku akifunga jumla ya mabao 136 katika mashindano yote. Katika kipindi chake akiwa Sundowns, alifunga mabao 20 kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ya CAF, akionyesha kiwango bora na kuwa tishio la mara kwa mara katika mashindano hayo makubwa ya vilabu barani Afrika.
Mshambuliaji huyo alikuwa amebakiza mabao nane pekee kufikisha mabao 100 kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini, baada ya kumaliza akiwa amefunga mabao 92.
Tangu alipojiunga na Sundowns akitokea Highlands Park mwaka 2020, Shalulile mwenye umri wa miaka 32 alikua kwa kasi na kuwa mmoja wa wafungaji wa kutegemewa zaidi barani Afrika.
Uwezo wake wa kujitengenezea nafasi, bidii uwanjani na umaliziaji mzuri ulimfanya kuwa mhimili muhimu wa kikosi cha Sundowns kilichotawala soka la Afrika Kusini huku kikibaki mshindani wa kudumu katika mashindano ya vilabu ya CAF.