National News

DC MWAKISU AZITAKA NGO'S KUFANYA KAZI KWA UAMINIFU NA UADILIFU

Tarehe: 24 Jul, 2026


Mashirika na Taasisi zisizo za kiserikali kutoka Wilaya ya Kasulu, Mkoani Kigoma, vimetakiwa kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu katika kutoa huduma kwa wananchi ili kuongeza uwajibikaji, kujenga imani ya jamii, na kuchangia maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu wakati akifungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, ambapo amesema kuwa katika kuhakikisha maendeleo endelevu, taasisi na mashirika vinatakiwa kuzingatia uaminifu katika shughuli zao.

Nae, Kaimu Msajili wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Godfrey Jeremiah amewataka wadau wa mashirika mbalimbali kutokuwa na utaratibu wa kuanzisha mashirika kwa kutegemea wafadhili pekee na badala yake watengeneze vyanzo vitakavyo wasaidia kupata mapato endapo ikitokea changamoto ya upatikanaji wa wafadhili. 

Kwa upande wao, baadhi ya wadau wa mashirika na taasisi mbalimbali waliohudhuria katika kikao hicho wameeleza kuwa uaminifu katika utoaji wa huduma ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha wanapata wafadhili, hivyo kuwawezesha kupiga hatua katika shughuli za maendeleo, huku wakiwahimiza wadau wengine kufanya kazi kwa uadilifu kwa maendeleo endelevu