National News

AHUKUMIWA JELA MIAKA 30 KWA KUKUTWA NA BANGI

Tarehe: 24 Jul, 2026


Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Lindi, Julai 23, 2026, imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela Rashid Mohamed Mtala (33), mkazi wa Nanyanje Manispaa ya Lindi, baada ya kupatikana na hatia kwa kosa la kupatikana na dawa za kulevya aina ya bangi.


Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Wilaya ya Lindi, Mheshimiwa Muyonga Bugendako Magara, baada ya Mahakama kujiridhisha kuwa upande wa Mashtaka umethibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa pasipo kuacha shaka.

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa Mahakamani, Rashidi alikamatwa Machi 5, 2026, majira ya saa 11:45 jioni katika eneo la Muhimbili, Barabara ya Jangwani, Wilaya ya Lindi, na askari waliokuwa doria. Wakati wa ukamataji huo, mtuhumiwa alikutwa akiwa amehifadhi misokoto 1,511 ya bangi yenye uzito wa kilogramu 1.26, iliyokuwa imewekwa ndani ya mfuko wa Super Sembe wa "Sulphate" na mfuko mdogo wa "Nailon".

Baada ya kukamatwa alipelekwa Kituo cha Polisi Lindi kwa hatua za kisheria. Mshtakiwa alifikishwa Mahakamani Mei 20, 2026, ambapo alisomewa shtaka linalomkabili na kulikana. Katika usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi sita na vielelezo vinne vilivyoiwezesha Mahakama kufikia uamuzi wa kumtia hatiani.

Upande wa mashtaka uliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Hilali Hamza.