National News

RC SIRRO AWATAKA MADIWANI KASULU KUPAMBANA NA WAHAMIAJI HARAMU

Tarehe: 23 Jul, 2026


Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amewataka madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki katika jitihada za kutokomeza tatizo la wahamiaji haramu katika maeneo yao.


Akizungumza katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kilichoitishwa kujadili hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Balozi Sirro amesema kuwa kila mhamiaji anayetarajia kuingia au kuishi nchini anapaswa kufuata sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa ili kuhalalisha uwepo wake.

Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya viongozi wa ngazi mbalimbali na wananchi ni muhimu katika kudhibiti uhamiaji haramu, ambao unaweza kuhatarisha usalama na maendeleo ya jamii.

Kwa upande wao, baadhi ya madiwani waliohudhuria kikao hicho wameahidi kuunga mkono juhudi za serikali katika kukabiliana na tatizo la wahamiaji haramu, huku wakiviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo ya mipakani ili kuzuia wahamiaji hao kuingia nchini kinyume cha sheria.