National News

ULEGA AAHIDI UJENZI WA BARABARA KIWANGO CHA LAMI KAKONKO

Tarehe: 23 Jul, 2026


Serikali imeahidi kujenga kwa kiwango cha lami barabara muhimu katika Makao Makuu ya Wilaya ya Kakonko, mkoani Kigoma, kufuatia ombi lililowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Kakonko, Alan Mvano, la kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara inayounganisha eneo la mjini, Ofisi za Halmashauri na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.

Mbunge Mvano alisema ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha lami utarahisisha shughuli za kiutawala, kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na kuongeza hadhi ya Makao Makuu ya Wilaya ya Kakonko.

Akijibu ombi hilo, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema Serikali imekubali kutekeleza mradi huo na kwamba tayari ametoa maelekezo kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma kuanza taratibu za utekelezaji wa ujenzi wa barabara hizo.

Waziri Ulega alieleza kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo utasaidia kuimarisha huduma za Serikali, kurahisisha usafiri na usafirishaji, pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Wilaya ya Kakonko.