WAANDISHI WA HABARI KIGOMA WAPEWA MAFUNZO KURIPOTI NA KUZUIA EBOLA
Tarehe: 22 Jul, 2026
Katika kuimarisha juhudi za Serikali za kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa Ebola, waandishi wa habari mkoani Kigoma wamepatiwa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo kuhusu namna ya kuripoti kwa usahihi ugonjwa huo, kutoa elimu kwa umma na kuchangia katika hatua za kinga dhidi ya mlipuko unaoweza kujitokeza.
Mafunzo hayo yameendeshwa na Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma Mkoa wa Kigoma, Abed Michael, kwa kushirikiana na timu kutoka Wizara ya Afya. Yamelenga kuwawezesha waandishi wa habari kuelewa dalili za Ebola, njia za maambukizi, hatua za kujikinga pamoja na umuhimu wa kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapobaini mtu mwenye dalili zinazoweza kuashiria ugonjwa huo.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Abed amesema kuwa kutokana na kuwepo kwa visa vya Ebola katika baadhi ya nchi jirani ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ni muhimu wananchi kuendelea kupewa elimu sahihi kuhusu ugonjwa huo ili kuongeza umakini na ushirikiano katika kuzuia maambukizi.
Ameeleza kuwa baadhi ya dalili za Ebola ni pamoja na homa kali, kutokwa na damu katika sehemu mbalimbali za mwili, kuvimba au kutokea vipele mwilini, maumivu makali ya kichwa, pamoja na kuharisha na kutapika kwa wakati mmoja. Hata hivyo, amesisitiza kuwa dalili hizo zinaweza kufanana na magonjwa mengine, hivyo ni muhimu kutowahukumu wagonjwa bali kuwafikisha katika vituo vya afya kwa uchunguzi na uthibitisho wa wataalamu.
Aidha, imeelezwa kuwa ugonjwa wa Ebola huambukizwa kupitia kugusana na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa, kama vile damu, mate, matapishi, kinyesi na machozi, pamoja na kugusa mizoga ya watu au wanyama waliokufa kutokana na ugonjwa huo, hasa ikiwa kuna michubuko au majeraha kwenye ngozi.
Abed ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa mapema kwa viongozi wa maeneo yao au vituo vya afya wanapobaini mtu mwenye dalili zinazotia shaka, huku akisisitiza kuwa ni wataalamu wa afya pekee wenye mamlaka ya kuthibitisha iwapo mgonjwa ana Ebola baada ya vipimo rasmi kufanyika.