RAIS SAMIA AMEIMARISHA MIUNDOMBINU MKOA WA KIGOMA - ULEGA
Tarehe: 22 Jul, 2026
Serikali imesema Mkoa wa Kigoma umepata mageuzi makubwa ya miundombinu ya barabara katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hatua iliyorahisisha usafiri, kupunguza gharama za usafirishaji na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Akizungumza mkoani Kigoma, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema ndani ya miaka mitano serikali imejenga kilomita 335 za barabara za lami, kiwango ambacho kimevuka ujenzi uliofanyika katika takribani miaka 60 tangu Tanzania ipate Uhuru.
Ulega amesema serikali pia imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 600 katika utekelezaji wa miradi tisa ya kimkakati ya barabara mkoani humo, ambayo imelenga kuunganisha maeneo mbalimbali, kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa pamoja na kufungua fursa za biashara, uwekezaji na utalii.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kiza Mayeye, amesema uboreshaji wa miundombinu ya barabara unaifanya Kigoma kuendelea kuwa lango muhimu la uchumi wa Tanzania. Ameeleza kuwa barabara hizo zimeboresha maisha ya wananchi kwa kupunguza muda wa safari, kushusha gharama za usafirishaji na kurahisisha shughuli za biashara katika maeneo mbalimbali ya mkoa.