Halmashauri ya Mji wa Kasulu mkoani Kigoma imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 4 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato ya ndani ya halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 5 kutoka kiasi kilichokasimiwa.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Mji Kasulu Mwl. Vumilia Simbeye wakati akizungumza na vyombo vya Habari, ambapo ameeleza kuwa halmashauri hiyo imefanikisha hayo kutokana na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa kuhakikisha wanatoa elimu kwa wafanyabiashara na wajasiriamali ili kutambua umuhimu wa kulipa kodi kwa wakati.
Aidha, Mwl. Simbeye amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2026/27 lengo ni kukusanya zaidi ya bilioni 4.1 huku akibainisha tayari mikakati mbalimbali imewekwa ili kuhakikisha hilo linafikiwa.
Ameongeza kuwa mapato yanayokusanywa yamekuwa yakichangia kuboresha utoaji huduma za kijamii pamoja na kuwezesha utekelezaji wa mpango wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, hatua inayosaidia wananchi kujiongezea kipato na kujikwamua kiuchumi.