UJENZI SGR TABORA -KIGOMA KUIMARISHA USAFIRISHAJI NCHINI
Tarehe: 20 Jul, 2026
#HABARI: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Tabora hadi Kigoma ni hatua muhimu katika kuimarisha usafiri na usafirishaji nchini pamoja na kuunganisha shughuli za kiuchumi za Mkoa wa Kigoma na masoko ya ndani na nje ya nchi.
Rais Samia amesema hayo leo Jumatatu Julai 20, 2026 mkoani Kigoma wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo na uzinduzi wa meli nne za mizigo katika Bandari ya Kigoma, akieleza kuwa Serikali imeanza kutekeleza ahadi ya kuifanya Kigoma isiwe mwisho wa reli bali kuwa sehemu ya kuunganisha fursa za biashara na uwekezaji.
Amesema mradi wa SGR Tabora hadi Kigoma wenye urefu wa takribani kilometa 506 unagharimu dola za Marekani bilioni 2.74, sawa na Shilingi trilioni 7.4, na utakapokamilika utaunganisha Kigoma na mikoa ya Tabora, Dodoma, Morogoro hadi Dar es Salaam pamoja na mtandao wa reli unaoelekea Mwanza.
Vilevile amesema, kukamilika kwa reli hiyo kutawezesha mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kufika Kigoma kwa haraka na kwa uhakika, huku wafanyabiashara na wajasiriamali wakinufaika kupitia kupungua kwa muda na gharama za usafirishaji.
Ameeleza kuwa mnyororo wa shughuli zitakazochochewa na mradi huo utazalisha fursa za ajira kwa vijana wa Kigoma katika maeneo mbalimbali ikiwemo usafirishaji, maghala, huduma za hoteli, matengenezo ya mitambo na shughuli nyingine zitakazotokana na uwepo wa reli hiyo.
Rais Samia amesema Serikali inaendelea kujenga miundombinu ya usafiri na usafirishaji kwa lengo la kuifungua Tanzania kibiashara na kiuwekezaji, huku akisisitiza kuwa kila reli, bandari, barabara na kiwanja cha ndege kinachojengwa kinaunganisha maeneo ya ndani na fursa za masoko.
Amesisitiza kuwa SGR Tabora–Kigoma ni sehemu ya jitihada za kuimarisha nafasi ya Tanzania katika usafirishaji wa kikanda, huku Kigoma ikitarajiwa kunufaika kutokana na nafasi yake ya kimkakati inayoiunganisha Tanzania na nchi jirani.
Sikiliza MAIN FM kupitia 91.7 Mhz Kigoma, Kasulu, Uvinza, Buhigwe.
Pia tufuatilie kwenye Mitandao ya Kijami, Instagram, Facebook, TikTok, na Youtube Main FM Tanzania pia tusikilize kupitia www.mainfm.co.tz pia Radio Box na Radio Garden tafuta Main FM
Fuatilia Youtube Chaneli Yetu ya Main FM Tanzania.